Madhara Ya Kidini Na Kimaadili
1- Kupitwa na vipindi vya Swala au kutokuswali kabisa;
2- Kupoteza muda, katikati ya mchana wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani watu huhangaika kutafuta Mirungi na kucheza bao, keramu, dhumna, kutazama mipira na sinema. Jambo la kwanza baada ya futari, watu huanza kusaga Mirungi. Hakuna Swala za usiku, hakuna ‘Ibada nyingine yoyote, hata Swala ya Alfajiri huwapita wengi kwa sababu Shaitwaan wa Mirungi huwaambia wakalale muda mchache tu kabla ya Swalah ya Alfajiri! Kuamka kwao ni mchana au Alasiri, Ramadhani inakuwa haina uzito wowote kwa maisha ya mla Mirungi.
3- Mchanganyiko baina ya wanaume na wanawake.
4- Uongo, Hii ni kawaida kwa wengi ili wafikie malengo ya kupata wakitakacho; ima kudanganya wengine kwa kuwakopa pesa za kununulia Mirungi na kisha hawarejeshi madeni hayo. Aidha wanapokopa husingizia matatizo makubwa waliyonayo wao au jamaa zao kama maradhi, matibabu, ada za shule, n.k. ili waweze kukubaliwa kupata mikopo. Aghlabu wanapokopa hawasemi ukweli kua wanataka pesa za kununulia Mirungi; maana hakuna atakayewakopesha kwa kusema kwa ukweli.
5- Usengenyaji, Vikao vingi vya watumiaji Mirungi huwa ni mazungumzo ya kidunia, mipira, filamu, kujadili mambo ya siasa, jamii, Na kujadili maisha ya watu, maingiliano ya kindoa, Na wao kwa wao kutoa siri zao za ndani na kutaja maovu yao waliyowahi kuyafanya.
6- Uropokaji, uchache wa adabu, ujuaji wa kila kitu, mtumiaji wa Mirungi akiongelea siasa basi hakuna mwanasiasa kama yeye, akija kwenye mpira wa miguu na hususan ligi maarufu za duniani kama Uingereza, Uhispania, Ujerumani na Ufaransa basi hakuna anayeichambua ligi hizo kama yeye… na mtihani mkubwa ni kua hata mas-ala ya Dini wao pia ni wajuzi wakioongelea Historia na kwanini fulani aliuliwa na wangapi waliritadi baada ya Mtume?! Na kwanini fulani walikuwa hawastahiki Ukhalifa walimdhulumu fulani n.k.!!
7- Upungufu wa hayaa na aibu.
8- Kupoteza muda mkubwa katika vikao hivyo.
9- Kuomba omba, Wengi huwa hawana uwezo wa kununua Mirungi kukidhi mahitaji ya uraibu wao, na hivyo kuwapelekea kuwa waombaji kwa wengine pesa za kununulia au uombaji wa Mirungi kwa walaji wenzao.
10- Kuharibiwa itikadi zao, Kutokana na ripoti nyingi zaeleza kua Mkoa wa Arusha vijana wengi wamebadili itikadi zao za Dini baada ya kujiunga na uraibu huo na kushiriki vikao vyake. Ndani ya vikao hivyo kuna kundi la wakongwe ambao wameweza kuwashawishi vijana kutoka katika itikadi waliyozaliwa nayo. Imefikia hali ya kusikitisha sana kwa kuona kundi kubwa la watu likiwa limekaa barazani likicheza Dhumna (Domino) na huku Swala ya Jamaa ikisimamishwa, na wala watu hawana wasiwasi tena huku wakifanya zogo na kelele za kuzipigisha kete zao kwa nguvu kama vile wanashindana na sauti ya Mnadi Swala.
12- Haki za kifamilia kukiukwa, Haki za kinyumba; waume wengi hawatimizi haki za nyumba zao kwa kukesha nje ya nyumba zao, Na kudhoofika nguvu zao za kiume na pia kumaliza haraka wanapofanya tendo la ndoa na hivyo kusababisha wake kukosa haki za msingi, Aidha Haki za watoto kutotekelezwa kwa kuwa walaji wengi wa Mirungi hawafanyi kazi, na wanaofanya kazi hutumia gharama nyingi kwenye ulaji wa Mirungi, hivyo hakupatikani matumizi nyumbani au matumizi kubanwa na haki kutotimizwa. Walaji wengine hulelewa watoto wao na wakwe zao au wazazi wao, Kwa sababu hiyo watoto uupoteza mapenzi ya mzazi (Baba).
13- Kutoka nje ya ndoa, Baadhi ya walaji wa Mirungi wanakuwa si waaminifu kwenye ndoa zao, kadhalika baadhi ya wake wanashindwa kuvumilia kuwa wapweke kila mara kwa kuwa waume zao hukesha nje ya nyumba zao, Hivyo hupelekea wake hao kukosa uvumilivu na kwa kuzidiwa kwao na matamanio yao kunawapelekea kukidhi mahitaji yao pengine, Hatima ya mambo hayo ni Talaka kuzidi katika jamii kwa sababu tulizotaja hapo kabla, Wake wengi hushindwa kuvumilia katika ndoa zao na kuamua kudai talaka zao kwa sababu hizo.
14- Walaji wa uraibu huu hukesha kuorodhesha mambo watakayoyafanya siku ifuatayo na kuyatekeleza, na kuendelea katika hali hiyo kila mara bila ya mafanikio yoyote.
15- Wengine husingizia eti wanakesha kwa ajili ya Ibada, lakini ni aina gani ya Ibada inayofanyika wakati mashavu yametuna kwa kujaa majani hayo?